Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Marekani yatangaza msaada wa dharura kukabiliana na tishio la viwavijeshi nchini

Februari 23, 2006

Balozi wa Marekani nchini Tanzania Michael Retzer ametangaza hatua za dharura kuisaidia Serikali ya Tanzania kudhibiti mlipuko wa viwavijeshi unaotishia kuleta madhara nchini. Balozi Retzer ameahidi kutoa mara moja kiasi cha dola 50,000 kusaidia juhudi za dharura za kupambana na tishio hilo hapa nchini. Hatua ya Marekani inatokana na ombi alilolitoa Waziri Mkuu Edward Lowassa kwa wahisani kuisaidia Serikali ya Tanzania kukabiliana na mlipuko huo wa viwavijeshi, na pia kutokana na tathmini iliyofanywa na mtaalamu wa Marekani ambaye wiki iliyopita alitembelea maeneo yaliyoathirika na kusema kwamba, mlipuko huo ni mbaya zaidi kuliko iliyowahi kutokea. Baada kipindi kirefu cha ukame, viwavijeshi hivi sasa vinaelekea kaskazini kwa kasi kubwa kufuatia kunyesha kwa mvua. Zaidi ya hekta 63,000 za mazao zimevamiwa na viwavijeshi nchini Tanzania peke yake, na vinatishia kuingia Burundi, Rwanda, Kenya na kaskazini zaidi katika wiki chache zijazo (mwanzoni mwa mwezi wa Machi).

Kitengo cha kutabiri uvamizi wa viwavijeshi - Armyworm Forecasting Services (AFS) cha Wizara ya Kilimo, Chakula na Masoko, kina vituo takriban 85 nchini kote vyenye mitego ya kunasa nondo (moths). Taarifa kutoka kwenye vituo hivi zinasaidia kutoa utabiri wa kuaminika. Nondo wa viwavijeshi wananaswa kwa wingi sana na ukubwa wa eneo lililoathirika nchini Tanzania unazidi kuongezeka kwa kasi kubwa, tangu viwavijeshi walipoonekana mwanzoni mwa Januari 2006. Wizara ya Kilimo, Chakula na Masoko imebainisha maeneo makubwa yaliyoathirika katika mikoa ya kusini na kati. Aidha kizazi cha pili cha viwavijeshi kimeanza kuzaliana na hivyo kuifanya hali iwe mbaya zaidi.

Serikali ya Tanzania pamoja na wananchi vijijini imekuwa ikichukua hatua kudhibiti mlipuko huo, lakini kufikia Februari 17, chini ya asilimia 10 ya hekta 63,000 za mashamba yaliyoathirika (bila ya kuhesabu mbuga) zimeweza kupuliziwa dawa za wadudu. Kuenea kwa viwavijeshi hao kuelekea kaskazini hakuzuiliki, na kunayaweka mazao yaliyopandwa hivi karibuni katika hatari kubwa. Wiki iliyopita, Waziri Mkuu Lowassa alitoa ombi la msaada wa dharura kutoka kwa wahisani, kwa sababu mlipuko huu ni mkubwa kuliko iliyowahi kutokea na unazidi uwezo wa nchi kukabiliana kikamilifu na janga hilo.

Tarehe 22 Februari 2006, Balozi Retzer alipeleka taarifa rasmi mjini Washington kwamba mlipuko huo wa viwavijeshi ni janga linalohitaji kushughulikiwa kwa haraka. Taarifa hii ilisababisha kitengo cha kushughulikia maafa katika shirika la misaada la USAID, Office of Foreign Disaster Assistance, kuchukua hatua, ikiwa ni pamoja na kutoa msaada wa dola 50,000 kukabiliana na janga hilo hapa nchini. Balozi Retzer anatoa mwito kwa wahisani wengine kujitokeza haraka na kuunga mkono juhudi hizi za kuhakikisha kwamba Serikali ya Tanzania inaweza kudhibiti kikamilifu na kwa haraka janga hilo la mlipuko wa viwavijeshi.

- Translation -
This content is also available in English