Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Mkurugenzi wa Chuo cha Diplomasia kujifunza sera ya nje ya Marekani

Januari 24, 2007

Mkurugenzi wa Chuo cha Diplomasia, Prof. Abillah Omari, yuko Marekani kushiriki kwenye ziara ya mafunzo ya wiki tatu kuhusu sera ya nje ya Marekani, ambayo itafanyika kuanzia Januari 25 mpaka Februari 15, 2007.

Ziara hiyo ya mafunzo ni sehemu ya mpango maarufu unaopeleka viongozi kutoka nchi mbalimbali kuitembelea Marekani, International Visitor Leadership Programme, ambao unasimamiwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, kwa niaba ya wananchi wa Marekani. Lengo la mpango huo ni kuwakutanisha kitaaluma wananchi wa Marekani na wenzao wa Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ubalozi wa Marekani jijini Dar-es-Salaam, lengo la ziara hiyo ni kufafanua mchakato wa maamuzi ya sera ya nje ya Marekani; kuchunguza mchakato wa kubuni, kuelezea na kutekeleza sera ya nje katika mfumo wa demokrasia wa Marekani; kutathmini kipaumbele na malengo ya sera ya nje ya Marekani; na pia kuchunguza msimamo wa Marekani kuhusu masuala haya.

Prof. Omari ataungana na washiriki wengine 22 kutoka nchi mbalimbali, na ziara hiyo itawapeleka katika miji kadhaa nchini Marekani, ikiwemo Washington, D.C.; New York; El Paso, Texas; na au Indianapolis, Indiana; Lincoln, Nebraska; au Springfield, llinois; ambako washiriki watagawanyika katika makundi matatu.

Wakati wa ziara hiyo, washiriki watapata picha ya mfumo wa shirikisho wa serikali ya Marekani, wajibu wa taasisi za serikali kitaifa, wajibu wa taasisi za sera na utetezi, na diplomasia ya kiraia. Mada nyingine ni pamoja na wajibu wa asasi zisizo za kiserikali katika kuchambua sera ya nje, utatuzi na elimu kuhusu migogoro, wajibu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, haki za binadamu pamoja na wajibu wa vyombo vya habari.

Akiongea kuhusu ziara hiyo, Prof. Omari alisema anakwenda Marekani akiwa na matumaini na matarajio makubwa, kwa sababu mara nyingi amewahi kuulizwa atoe maoni yake kuhusu sera ya nje ya Marekani.

“Nimewahi kujifunza masuala ya sera ya nje, lakini nilikuwa bado sijaiangalia Marekani kwa makini. Nimekuwa nikishangazwa na sera ya nje ya Marekani, ambayo ninaiona kama ni pana na yenye sura nyingi, alisema Prof. Omari. “Kwangu mimi, hii ni fursa kujifunza, na ikiwezekana kuondoa baadhi ya mashaka niliyo nayo. Ninafurahi sana kwamba tutakuwa na muda wa kujifunza ‘diplomasia ya kiraia.’ Kama mkufunzi wa wanadiplomasia, ninafikiri nitagundua mambo fulani kuhusu suala hili,” aliongezea.