Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Makala ya Washington File

Marekani yaunda Kamandi mpya ya Afrika kuratibu shughuli za kijeshi

Februari 07, 2007

Washington – Wizara ya Ulinzi ya Marekani inaandaa makao makuu ya kamandi mpya ya Afrika (U.S. Africa Command), itakayojulikana kama AFRICOM, ambayo itakuwa ikiratibu maslahi yote ya kijeshi na kiusalama ya Marekani barani kote, utawala wa Bush ulitangaza February 6.

“Kamandi hii mpya itaimarisha ushirikiano wetu na Afrika katika masuala ya usalama na kuanzisha fursa mpya za kuinua uwezo wa washiriki wetu barani Afrika,” alisema Rais Bush kwenye taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Marekani (White House). “Kamandi ya Afrika itaimarisha juhudi zetu kuleta amani na usalama kwa watu wa Afrika na kufanikisha malengo yetu ya pamoja ya kuleta ustawi na kuchochea maendeleo katika maeneo ya afya, elimu, demokrasia, na uchumi barani Afrika.”

Mpaka sasa, shughuli za kijeshi za Marekani barani Afrika zilikuwa zimegawanywa kati ya Kamandi ya Ulaya, Kamandi ya Kati, na Kamandi ya Pacific. Waziri wa Ulinzi wa Marekani Robert Gates alisema, ugawaji huu wa majukumu ni “mpango uliopitwa na wakati kutoka enzi za Vita Baridi (Cold War).”

Kuundwa kwa AFRICOM “kutatuwezesha kuwa na msimamo thabiti na wenye ufanisi zaidi kuliko mfumo wa hivi sasa wa kuligawa bara la Afrika kati ya kamandi za kanda mbalimbali,” alisema Gates February 6, mbele ya Kamati ya Majeshi ya Bunge la Seneti (Senate Armed Services Committee).

Bush ametoa amri ya kuundwa kwa kamandi ya AFRICOM ifikapo September 30, 2008. Wakati huo, kamandi hiyo itakuwa ikiongozwa na jenerali mwandamizi mwenye kiwango cha nyota nne, ambaye atakuwa na hadhi sawa na makamanda wenzake wanaoongoza kamandi zingine za Marekani ulimwenguni kote. Katika taarifa yake iliyotolewa na Ikulu ya Marekani, Bush alisema kwamba Marekani ina mipango ya kushauriana na viongozi wa Afrika “kujua fikra zao kuhusu jinsi gani kamandi ya Afrika inaweza kuitikia changamoto za kiusalama.” Alisema pia kwamba, Marekani “itashirikiana kwa karibu na washiriki wenzetu katika kuamua sehemu inayofaa kuwa makao makuu ya kamandi hiyo mpya barani Afrika.

Timu inayoandaa kuundwa kwa kamandi hiyo mpya inafanya kazi kwenye ofisi zake za muda huko Stuttgart, Ujerumani, ambayo pia ndiyo makao makuu ya Kamandi ya Marekani Ulaya. Hata hivyo, Wizara ya Ulinzi ingependa kuweka makao makuu ya kamandi mpya ya AFRICOM kwenye nchi ya Kiafrika.

Maafisa wameanza kujadiliana kuhusu sehemu ya kuweka makao makuu ya kudumu ya kamandi hiyo mpya, na wanatathmini ni majeshi aina gani yatapangiwa kwenye kamandi ya AFRICOM, alisema Navy Rear Admiral Robert Moeller wa Kamandi ya Kati, ambaye ni mkurugenzi wa timu inayoandaa kuundwa kwa kamandi ya AFRICOM.

Wizara ya Ulinzi hutumia kamandi zake za kanda kuratibu maslahi ya kijeshi ya Marekani ulimwenguni kote. Maafisa waandamizi wa Marekani hufanya kazi kama wanadiplomasia na, inapolazimu, kama makamanda wa vita kwenye kanda husika. Hivi sasa, Kamandi ya Kati inaratibu shughuli za kijeshi Mashariki ya Kati, Pembe ya Afrika na Asia ya Kati; Kamandi ya Ulaya inaratibu eneo kubwa la nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara na Ulaya; Kamandi ya Kaskazini inaratibu Amerika ya Kaskazini; Kamandi ya Kusini inaratibu Amerika ya Kusini, Amerika ya Kati na eneo la Caribbean; na Kamandi ya Pacific inaratibu Asia ya Mashariki na Asia ya Kusini, pamoja na visiwa vya Bahari ya Hindi, nje ya pwani iliyo kusini mwa mashariki ya Afrika.

Hatimaye, Kamandi mpya ya AFRICOM itahusisha eneo zima la bara la Afrika, isipokuwa Misri, ambayo iko chini ya Kamandi ya Kati. AFRICOM pia itahusisha visiwa vya Cape Verde, Equatorial Guinea, Sao Tome na Principe, pamoja na visiwa vilivyo katika Bahari ya Hindi vya Comoro, Madagascar, Mauritius na Seychelles.

Kuundwa kwa AFRICOM kutaiwezesha Wizara ya Ulinzi kuratibu vizuri zaidi shughuli zake barani Afrika, na pia kusaidia kuratibu kazi za taasisi zingine za Serikali ya Marekani, hususan Wizara ya Mambo ya Nje na shirika la misaada la USAID, alisema Moeller, mkurugenzi wa timu inayoandaa kuundwa kwa AFRICOM.

Maafisa wa Serikali ya Marekani wataweza pia “kufanya kazi kwa karibu na washiriki wetu barani kote,” alisema Moeller, na kuongeza kwamba, kwa muda mrefu, nchi nyingi za Kiafrika zimekuwa zikiomba kuanzishwa kwa kamandi pekee itakayolenga masuala ya Afrika.

Balozi Robert Loftis, mpatanishi mwandamizi kwenye Wizara ya Mambo ya Nje alisema kwamba, tayari kamandi za kijeshi za Marekani na taasisi zingine za serikali zimekuwa zikishirikiana na nchi za Afrika kufanya kazi mbalimbali. Kuundwa kwa AFRICOM, alisema Loftis, “kunamaanisha kwamba, shughuli zote ambazo zinafanyika mpaka sasa zitakusanywa pamoja na kuwekwa chini ya kamandi moja.”