Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Kiswahili By-Liner

SIKU YA MALARIA AFRIKA – Na Michael L. Retzer

Aprili 25, 2007

Leo tunaadhimisha siku ya Malaria Afrika duniani kote. Mbu waenezao malaria wameshamiri kutokana na hali ya hewa ya Afrika, kusini mwa jangwa la Sahara na kuziacha familia, vijiji na jamii zikiwa zimeharibikiwa. Ingawaje imekuwa ikikubalika kama hali ya kawaida katika maisha – kuchaga kwa tishio hilo kunavumilika – yatubidi kuishinda hali hiyo sasa. Kuangamiza malaria ni wito na lengo linafikiwa.

Leo tuna matumaini mapya katika vita dhidi ya ugonjwa huu uliokwisha ua watu wengi, hasa wanawake na watoto Tanzania nzima na majirani zetu katika bara hili. Mpango wa rais wa kupambana na malaria (PMI) – wa dola bilioni 1.2 zilizoahidiwa kutolewa na Marekani kupunguza kiasi cha nusu ya vifo vitokanavyo na malaria hapa na nchi nyingine 14 zinazoshambuliwa vikali na ugonjwa huo—umepiga hatua kubwa.

PMI imepata mafanikio makubwa katika kupambana na ugonjwa wa malaria. Msaada wa watu wa Marekani umewafikia takribani watu milioni 6 katika nchi tatu za Afrika katika mpango wa mwanzo pamoja na Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi hizo. Mwaka huu, zaidi ya watu milioni 30 watanufaika na tiba ya kuokoa maisha na hatua za kinga kutokana na PMI kupanuka kutoka nchi tatu hadi saba.

Mpango huu wa Marekani unahakikisha dawa mpya zinazofaa zinafika katika vituo vya afya vijijini na kuondoa matibabu yasiyofaa; kuwapatia kina mama wajawazito angalau dozi mbili itakayowalinda na watoto wao ambao hawajazaliwa; kusambaza vyandarua vyenye dawa inayodumu kwa muda mrefu vitakavyozuia kushambuliwa na mbu; na kunyunyuzia kiasi kidogo cha dawa katika kuta za ndani ya nyumba kuua mbu waenezao malaria.

Hii ni habari njema kwa Tanzania. Tutaweza kuipiga vita malaria kama vile wenzetu wa nchi za magharibi walivyofanikiwa katika miaka ya 1950 ugonjwa huo ulipokaribia kutokomezwa kabisa – hata katika hali ya joto la kadri au joto jingi kama tulilonalo hapa. Kumbuka kuwa ugonjwa huu unatibika na unazuilika. Kama Zanzibar imeweza kuthibitisha kwa kupunguza malaria Pemba kwa asilimia 87 mwaka 2006 ikilinganishwa na 2005, Tanzania itaweza kuondokana na malaria.

Ufumbuzi katika vita hii ni uamuzi wetu wenyewe, uwajibikaji kwa mtu mmoja mmoja na uongozi. Mosi, kila Mtanzania kwa kila usiku mwaka mzima awe ametundika na kulala ndani ya chandarua kilichotiwa dawa. Kama mbu hawakufikii, hawawezi kukung’ata na kukuambukiza malaria.

Pili, ukijihisi una malaria, nenda haraka kwenye kituo cha afya kilichokaribu upimwe na utibiwe na dawa mseto ya Artemisinin (ACT). Hii ni dawa bora iliyopo kwa tiba ya malaria. Zanzibar imekuwa ikitumia dawa hii kwa miaka mitatu na leo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Tanzania bara inazindua dawa iitwayo ‘ALU’. Dawa hiyo ya ALU itapatikana katika vituo vyote vya wizara hiyo vinavyohusika na ALU. Endapo utapatikana na vijidudu vya malaria na ukatibiwa na ALU, utapona haraka na damu yako yenye vijidudu vya malaria haitaathiri mbu wengine wenye vimelea vya malaria.

Tatu, kama ni mjamzito, mbali na kulala ndani ya chandarua chenye dawa kila usiku, pia pata dawa aina ya Sulfadoxine-Pyrimethamine (SP) kama sehemu ya huduma kwa wajawazito. Hii itaua vimelea vya malaria vinavyoweza kuwepo kwenye mwili ambavyo vinaweza pia kumdhuru mtoto ambaye hajazaliwa. Nne, shirikiana na familia yako na jirani zako kusafisha mazingira ili kupunguza mbu na inapowezekana, tumia dawa ya kunyunyuzia kuta za ndani.

Serikali ya Tanzania imeamua kulipa umuhimu mkubwa suala hili la afya kwa kushirikiana bega kwa bega na serikali pamoja na Mpango wa Taifa wa Kuzuia Malaria, Shirika la Afya Duniani, ‘Global Fund’, mashirika yasiyo ya kiserikali, mashirika ya dini na vikundi vingine vya kijamii. Kwa moyo wangu wote, ninazipongeza Wizara za Afya na Ustawi wa Jamii za Tanzania bara na Visiwani kwa programu zao nzuri za kupambana na malaria. Wahisani wengi, ikiwemo serikali ya Marekani kupitia PMI (Mwaka 2007 imetoa dola milioni 31 kwa ajili ya kuzuia, kudhibiti na kutibu malaria), inaunga mkono shughuli hizi. Mafanikio yatapatikana katika shughuli hizi za kupambana na malaria endapo Watanzania wote watashiriki kikamilifu.

Sasa tunazo nyenzo, elimu na vifaa, mafunzo pamoja na nia, na tunaweza kumshinda adui lakini tukitaka kupata mafanikio na kuweza kusitisha kuenea kwa ugonjwa huu, watu binafsi watoe kipamumbele kuzilinda familia zao na vijiji vyao. Hakuna tunu ambayo ni adimu kama afya. Kutoka Arusha hadi Zanzibar, lazima tuwe pamoja kusaidia majirani zetu. Tusipoteze nafasi hii tushinde vita ya kupambana na malaria. Kataa Malaria.


Michael L. Retzer ni Balozi wa Marekani nchini Tanzania